Na Marco Maduhu (ESKi Tanzania Alumni)
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizojaliwa utajiri wa rasilimali za madini, gesi asilia na mafuta. Utajiri huu ni kinyume na maisha halisi ya wananchi wake.
Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliweka Dira ya Rasilimali kuwa madini yanufaishe watanzania kwanza kupitia Azimio la Arusha. Hivyo, rasilimali zote zilizokuwa zinamilikiwa na watu binafsi hususani wageni zilirudishwa chini ya umiliki wa umma wa watanzania, na serikali ikiwa muangalizi mkuu.
Kutokana na changamoto za ujuzi, kukua kwa teknolojia pamoja na changamoto za kimitaji mwaka 1997, Serikali ilitunga Sheria ya Madini kukaribisha wawekezaji wakubwa kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza hapa nchini.
Hisia za watanzania walio wengi hususani wanaoishi karibu na maeneo ya uchimbaji ni kuwa baada ya kukaribisha wawekezaji miaka ya 1990, rasilimali zetu hususani madini, mafuta na gesi asilia hazinufaisha tena watanzania zaidi ya kunufaisha nchi/makampuni yaliyowekeza hapa nchini.
Mwaka 2010 Serikali ilifanya tena marekebisho ya sheria ya madini na kuweka masharti kwa wawekezaji, kuwa ajira, utoaji wa huduma mbalimbali ndani ya migodi wapewe kipaumbele wazawa (local content), pamoja na kuwajibika kwenye jamii kwa kushirikiana na jamii husika kuandaa kwa pamoja mipango, na kujenga miundombinu ya maendeleo kwenye vijiji/maeneo yanayozunguka migodi (Corporate Social Responsibility).
Mwaka 2015, rais wa awamu ya tano – Dr. John Pombe Magufuli akifuata nyayo za Mwalimu Nyerere, alizuia makinikia kutoka nje ya nchi, pamoja na kuibana migodi hususani kwenye maswala na utaratibu wa usafirishaji makinikia nje ya nchi, maamuzi hayo yalipelekea kutungwa kwa sheria mbili za utajiri wa rasilimali na maliasili ya nchi juu ya mamlaka ya kudumu ya Tanzania kwenye rasilimali zake (The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty) Act of 2017) na sheria ya upitiaji upya majadiliano ya mikataba (The Natural Wealth and Resource (review and negotiations of unconscionable terms) of 2017) kwa vitendo.
“Tanzania itaweza kunufaika na Rasilimali zake, endapo utekelezaji wa sera na sheria utazingatia maslahi mapana ya Taifa, na siyo kujali fedha tu (deals for Capital) na kuingia kwenye mikataba mibovu kila siku kwa sababu ya kuongeza mapato.” Akitolea mfano wa “Nchi kama Marekani ikipata Rasilimali ya Gesi au Mafuta kama ilivyopatikana Mtwara matumizi yao makubwa yatakuwa ya ndani tu, na ipo tayari kuagiza Gesi kutoka nje ya nchi, lengo ni kuweka mikakati ya kuwanufaisha, pamoja na vizazi vijazo,” Alisema mmoja wa wageni katika mafunzo ya misingi ya utetezi wa Jamii katika utawala wa sekta ya Madini, mafuta na gesi Tanzania.
Mafunzo ya “Misingi ya Utetezi wa Jamii katika Utawala wa Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi Tanzania” (Fundamentals of Community Led Advocacy in Mining, Oil and Gas Governance) kupitia program yake ya Extractive Sector Knowledge Transfer Incubator (ESKi Tanzania) yanatolewa kwa ushirikiano wa HakiRasilimali (Shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi ya uchechemuzi kwenye sekta ya Madini mafuta na gesi nchi Tanzania) pamoja na chuo cha Ms TCDC kilichopo jijini Arusha.
Mafunzo hayo yalihusisha washiriki takribani 23 kutoka makundi mbalimbali, yakiwamo Mashirika yasiyo ya kiserikali, vyama vya wachimbaji madini wanawake (TAWOMA), wachimbaji wadogo, wanasheria, pamoja na wanahabari, ambapo wanafanyakazi katika maeneo shughuli za madini, mafuta. na Gesi zinafanyika.
Mafunzo hayo yalifanyika ndani ya wiki mbili kuanzia Sept 21-Oktoba 2 na yaliyofanyika katika chuo cha Ms TCDC Jijini Arusha, yaliyokuwa na lengo la kupanua uelewa kwa washiriki hao juu ya dhana nzima ya uziduaji katika Sekta ya madini, mafuta na Gesi.
Makala hii naaandika nikiwa kama mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo, vitu ambavyo vilifundishwa na kujadiliwa viliongeza wino katika karamu yangu juu ya tafakari ya namna malengo ya Mwalimu Nyerere yanaweza kufikiwa katika kipindi cha sasa. Ili basi Rasilimali zinufaishe watanzania; Jambo la Muhimu ni uwepo na uwazi kwenye mikataba (Transparency), na uwajibikaji (Accountability) kwenye Sekta, huu ndio msingi kwa sababu watanzania watajua ni nini kimekubaliwa na mwekezaji, Pia uwazi utaongeza ushiriki wa watanzania hususani kwenye maamuzi juu ya rasilimali zao.
Pili, uwepo wa mkakati wakuwekeza kwa muda mrefu kwa ajili ya vizazi vya baadae, pamoja na kuzisimamia Sera na Sheria za madini kwa vitendo, ikiwamo kudhibiti uharibifu wa mazingira, ulipaji wa fidia kwa wakati na haki kwa wananchi ambao maeneo yao yanatwaliwa kupisha miradi.
Aidha jambo jingine ni kulisimamia suala la migodi au makampuni kuwajibika kwa wananchi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo (Social Cooperate Responsibility), pamoja na ulipaji sahihi Kodi ya ushuru wa huduma kwenye halmashauri husika (Service Levy) kulingana na uzalishaji halisi wa madini, mafuta na Gesi. CSR na ushuru wa huduma vinamchango kwenye maendeleo ya Jamii husika.